27 Septemba 2020 - 10:06
Rais Rouhani: Uwepo wa majeshi ya Marekani Asia Magharibi ni pigo kwa usalama na uthabiti wa eneo

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Iraq, Afghanistan na katika mataifa ya kusini mwa Ghuba ya Uajemi ni pigo kwa amani na uthabiti wa eneo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Rouhani amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Fuad Hussein, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq ambapo amesisitiza kwamba, ni jukumu la kila nchi kufanya hima na juhudi kwa ajili ya kuondoka majeshi ya Marekani katika eneo hili.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Tehran inauona uamuzi uliopasishwa na Bunge la Iraq wa kuondoka majeshi ya Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu kuwa hatua chanya na muhimu.

Rais Rouhani amebainisha pia katika mazungumzo yake na Fuad Hussein kwamba, Iran ikiwa na lengo la kusaidia umoja na mshikamano wa Iraq iko pamoja na serikali na wananchi wa nchi hiyo.

Aidha Rais Rouhani amekumbusha jinsi ambavyo Iran daima imekuwa ikiwaunga mkono wananchi na serikali halali ya Iraq na mfano wa wazi katika hilo ni msaada wa taifa hili kwa Iraq katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.

Kwa upande wake, Fuad Hussein Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq ameshukuru mno himaya na misaada ya Iran kwa serikali na wananchi wa taifa lake na kueleza kwamba, ana matumaini safari yake hii hapa nchini itapelekea kuhuishwa makubaliano yaliyofikiwa huko nyuma baina ya pande mbili.

342/